Jumatatu , 28th Mar , 2016

Wadau na mashabiki wa soka nchini Tanzania wamekuwa na maoni tofauti kufuatia hatua ya timu ya taifa ya Chad kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania tiketi ya kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) nchini Gabon mwaka 2017.

Kikosi cha stars kikifanya mazoezi nchini Chad kabla ya mchezo wa kwanza dhidi ya wenyeji wao hao.

Mashabiki na wadau wengi wa soka nchini hasa wale ambao walikuwa na shauku kubwa na hamu ya kukiona kikosi cha taifa stars kikiendeleza wimbi la ushindi mbele ya Chad hii leo, hali hiyo imekuwa tofauti mara baada ya kupatikana na taarifa kutoka shirikisho la vyama vya soka barani Afrika CAF kutanga kujitoa mashindanni kwa timu ya Chad iliyokuwa katika kundi G lenye timu za Misri, Nigeria pamoja na Tanzania.

Chad ambayo ujio wake nchini ulikuwa wa mashaka huku baadhi ya wadau wakitafsiri hali hiyo ni kama timu hiyo kufanya mambo yake kimya kimya kukwepa hujuma kama inavyokuwa kwa timu kutoka nchi za kiarabu zinakuwa na tabia ya kutoweka mambo yao hadharani.

Na Kufuatia hali hiyo shirikisho la soka barani Afrika CAF limeifungia Chad kushiriki michuano ya AFCON kwa msimu mmoja na kuitoza faini ya dola elfu 20 adhabu ambayo baadhi ya wadau hao wamesema ni ndogo ikilinganishwa na gharama ama athali kwa timu nyingine zilizocheza nao kama Taifa stars huku wakitafsiri hali hiyo kama ni mipango ya timu pinzani kupanga matokeo.

Wakiongea kwa masikitiko makubwa baadhi ya wadau hao wamesema adhabu za CAF zimekuwa ni ndogo sana ukilinganisha na athali zinazojitokeza baada ya kutokea kwa hali hiyo na wakasema ifikie wakati kama timu ama klabu inaona haitokuwa tayari kushiriki michuano flani basi isithibitishe ushiriki wake na pia adhabu itolewe kali kwa timu ambayo itajitoa katikati ya mashindano ikiwemo kufidia gharama za mchezo kwa timu walizocheza nazo.

Kwa uamuzi huo wa Chad kujitoa katika mbio hizo kutoka kundi G sasa kundi hilo linasalia na timu tatu zikiongozwa na Misri ambayo sasa itakuwa na alama nne kwa michezo miwili ikiifunga Tanzania [taifa stars] nyumbani mjini Cairo kwa bao 3-0 na juzi ikitoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Nigeria ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa na alama mbili baada ya kwenda sare na Misri na suluhu ya 0-0 na wenyeji wao Tanzania ambayo sasa itakuwa na alama moja baada ya suluhu hiyo na Nigeria na awali kupoteza kwa bao 3-0 ugenini dhidi ya Misri.

Kwa hali hiyo wadau hao wamelitaka shirikisho la soka nchini Tanzania kwakushirikiana na Serikali kuhakikisha kuhakikisha wanajipanga ili stars iweze kushinda michezo yote iliyobakia ukiwemo ule wa mwezi juni dhidi ya Misri utakaopigwa jijini Dar es Salaam na ule wa ugenini dhidi ya wenyeji Nigeria utakaopigwa Septemba mwaka huu.

Misri na Nigeria

Wakati huo huo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kuwarudishia fedha zao kesho Jumanne, wapenzi wa mpira wa miguu waliokuwa wameshakata tiketi za kushuhudia mchezo wa kundi G kati ya Tanzania v Chad jijini Dar es salaam.

TFF inawaomba washabiki wa mpira wa miguu waliokua wamekata tiketi za mchezo huo, kufika kesho Jumanne saa 5 kamili asubuhi katika vituo walivyonunulia wakiwa na tiketi zao ili waweze kurudishiwa fedha zao.

Zoezi la kuwarudishia fedha washabiki waliokuwa wameshakata tiketi za mchezo kati ya Tanzania v Chad litafanyika katika vituo vinne vilivyokua vikiuza tiketi siku ya Jumapili, hivyo wenye tiketi za mchezo huo wanaombwa kufika na tiketi zao ili waweza kurudishiwa fedha zao.

Aidha TFF inawaomba radhi watanzania na wapenzi wa mpira wa miguu kwa usumbufu uliojitokeza na kuwataka kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki ambacho wanasubiria taarifa zaidi kutoka CAF.

Chad imejiondoa jana katika kinyanganyiro cha kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) nchini Gabon mwaka 2017, ambapo iliku kundi G na timu za Misri, Nigeria pamoja na Tanzania.