Alhamisi , 15th Jun , 2023

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amevitaka vyama vya ushirika vya wakulima wa mazao mbalimbali, kujiendesha kibiashara ili kukuza uchumi wa ushirika na kujenga vyama imara vyenye kushiriki kwenye ushindani wa kibiashara.

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde

Mavunde ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Programu ya Taasisi ya ‘WE EFFECT’ ya  ‘Livehoods and Right to Food Program’ (LRF)Jijini Dodoma, ambapo moja ya vipaumbele vya Program hii ni maendeleo ya vyama vya Ushirika. 

"Kufuatia mpango wa Serikali wa kukuza kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030,Serikali imeweka mkakati wa kuimarisha maendeleo ya ushirika, kuhakikisha wakulima wananufaika na vyama vya ushirika na kuchangia kwenye sekta ya kilimo bila kuwepo na ubabaishaji," amesema Mavunde

Naibu waziri huyo ameongeza kuwa dhamira ya serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha kuwa Sekta ya kilimo inakua na mkulima ananufaika.

"Hivyo ushirika ninaotamani kuuona ni ule ushirika ambao utakuwa imara na ambao utashiriki moja kwa moja kwenye mnyororo wa uongezaji thamani wa mazao ya kilimo badala ya kuendelea kubaki wakusanyaji wa mazao ya wakulima," amesisitiza

Aidha ameongeza "Tumechoka kusikia ubadhirifu na sifa mbaya ya ushirika,tunataka sasa tuone ushirika imara utakaochochea uchumi wetu kwa kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo chini ya usaidizi mkubwa wa Benki ya Taifa ya Ushirika,".