Jumapili , 21st Mei , 2017

Mabasi 119 kati ya 185 ya kubeba wanafunzi yaliyofanyiwa ukaguzi jijini Dar es Salaam, yamebainika kuwa hayana sifa kutokana na ubovu na kuwa hatarishi kwa usalama wa watumiaji.

Mabasi hayo, maarufu kama ‘school bus’,  ambayo yamebainika kuwa hayana sifa, ni sawa na asilimia 64.3. Hadi sasa  yanashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kubainika kuwa yana makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ubovu.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Awadhi Haji, alisema  hadi juzi walikuwa wamefanya ukaguzi wa magari 185 na 119 kati ya hayo, yamebainika kuwa na makosa mbalimbali.

“Tunafanya ukaguzi wa ‘school bus’ kwa lengo la kuona ubora ili tujue kama yanakidhi viwango vya sheria za usalama barabarani. Hadi sasa tumekagua magari 185 kwa Mkoa wa Dar es Salaam 119 tumeyakuta yana upungufu mwingi ikiwamo ubovu wa bodi, matairi chakavu na viti vibovu,” alisema.