Jumatano , 26th Jul , 2017

Diwani wa kata ya Moita wilayani Monduli (CHADEMA) Edward Sapunyo amesema sababu ya kujiuzulu uongozi ni kutokana na vikwazo vilivyowekwa na chama chake wakati wa kufanya kazi na watendaji wa serikali, kitendo ambacho kinatafsiriwa kama  usaliti.

Moita ambaye amewawakilisha viongozi wengine wanaoendelea kujiuzulu mkoani Arusha wamesema wanalazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na kunyimwa fursa ya kushirikiana na viongozi na watendaji wa serikali kutatua kero za wananchi ikiwa ni pamoja na kutaka kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi anayoifanya.

Moita amesema anachokijua yeye ni kwamba pamoja na kuwa kiongozi kwenye chama cha Upinzani anapaswa kushirikiana na watendaji waliopo madarakani kutatua kero za wananchi lakini baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakiona kama ni usaliti.

“Moja ya jambo lililoniuma kuna mradi wa maji ambao nimehangaika nao tangu mwaka 2006 fedha zilipatikana na umekuwa unaendelea vizuri, lakini viongozi wangu wanaukwamisha usifikie tamati licha ya kuwa wananchi wameanza kutumia maji,”  alisema

Hata hivyo baadhi ya wananchi wa kata hiyo wametofautiana mitazamo juu ya kujiuzulu kwa madiwani hao ambapo baadhi yao wamefurahia na wengine wamesema wanachotaka ni kuona matatizo yao yanapata ufumbuzi na wanakuwa na maendeleo.

Kiongozi huyo amekabidhi barua yake ya kujiuzulu jana na kufikisha idadi ya madiwani waliojiuzulu mkoani Arusha kufika tisa.