Jumatano , 17th Sep , 2014

Kituo cha Sheria na haki za bianadamu (LHRC) kimemtaka rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete kusitisha bunge maalumu la katiba badala ya kuendelea kusubiri mpaka ifikapo Oktoba 4 mwaka huu.

Rais wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.

Akiongea jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa maboresho na uwezeshaji wa LHRC Lulu Urio, amesema kuwa rais ana nafasi kikatiba kusimamisha Bunge la katiba, kuleta mwelekeo mpya wa mchakato wa katiba na kuleta maridhiano ya mapungufu yaliyoonekana hapo awali ambayo yaliondoa maridhiano baina ya wajumbe wa UKAWA na wajumbe wengine.

Hata hivyo Bi. Urio amesema ni vyema mwenyekiti wa Bunge la katiba akasitisha vikao vyake ili upatikane muafaka baina ya pande zote mbili zinazokinzana na kuongeza kuwa Rasimu ya katiba inatoa kipindi cha mpito cha miaka minne kabla ya kuanza kutumia katiba mpya.

Wakati huo huo, Makamu wa rais wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutambua kuwa waandishi wa habari si adui hivyo basi wanapaswa kushirikiana nao.

Dk. Bilal ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua mkutano wa mashauriano kati ya Vyombo vya Habari na Vyombo vya Ulinzi, Usalama na Sheria ambao hata hivyo jeshi la polisi halikuweza kuleta mwakilishi wake kutokana na kukabiliwa na operesheni maalum.

Aidha Dkt. Balal amesema kuwa vyombo hivyo vielimishane kuhusu mipaka na maeneo ya ushirikiano ili kuondoa tofauti na mifarakano miongoni mwa vyombo hivyo ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara