Jumatano , 22nd Nov , 2017

Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Humphrey Polepole, amesema chama hicho kwasasa kimeweka misingi ambayo inawabana viongozi wasiotosheka lakini hakina tabia ya kuwasema vibaya wanachama wake wakihama.

Akiongea kwenye mahojiano na kituo kimoja cha habari Ndg. Polepole amesema kuwa Chama chao kinalinda misingi na Itikadi zake ambazo ni kuheshimu utu wa mtu pamoja na kuwatumikia raia hivyo kwa kiongozi ambaye hawezi kufanya hayo lazima atakimbia.

"Mimi kama Katibu wa Itikadi na Uenezi sijawahi kutoa tamko la kumsema vibaya mwanachama anayehama chama chetu kwasababu sio misingi na Itikadi zetu". Pia ameongeza kuwa ni dhambi kubwa kumhukumu mtu anapohama chama kimoja kwenda kingine.

“Hatuna tabia ya kuwasema vibaya wale wanaokihama chama, lakini tumegundua kwamba raia wa kawaida ndio wamekuwa na tabia ya kuwasema kwa sababu wanayaona matendo yao ya kutotosheka”, amesema Polepole.

Aidha Polepole amesisitiza kuwa CCM kwasasa imeweka misingi migumu itakayowabana wasiotosheka na wasio na kiasi ndio maana tumeamua kuweka sheria ya mtu mmoja, cheo kimoja. Sheria ambayo itawabana wenye kutaka vyeo vingi kwa wakati mmoja.