Ijumaa , 18th Aug , 2017

Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe amewataka watu wanaosimamia usalama wa nchi wawe makini kwa kile wanachokilinda lasivyo watajikuta wanaiteketeza nchi bila ya wao wenyewe kujijua.

Mbowe ameeleza hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliyofanyika leo na kusema kauli za kiongozi wa taifa ni za msingi pale zinapotolewa kulingana na Katiba, Sheria pamoja na mikataba ambayo kama nchi inaingia nayo kwa namna moja ama nyingine.

"Taifa lolote huongozwa na katiba pamoja na Sheria zake, na sheria huongozwa na kanuni. Tunapokuwa tunapuuza sheria zetu 'automatically' tunapuuza mikataba yetu. Mtawala anapofikili yeye yupo juu ya sheria, juu ya mikataba, mwisho wa siku wanaoumia ni watanzania. Kwa sababu Jumuiya na Jamii za Kimataifa inatambua sheria za Tanzania na wala haitambui kauli za viongozi wa taifa. Rais apongezwe pale anapofanya jambo jema lakini afanye jambo jema kwa misingi ya Sheria, Katiba na Kanuni ikiwemo na mikataba tuliyojiwekea", alisema Mbowe.

Pamoja na hayo, Mhe. Mbowe aliendelea kwa kusema "tusiwe wepesi wa kushangilia kila analolizungumza Rais kufikilia ni jambo jema hata kama lina sound vizuri katika masikio yetu. Lazima kama taifa tusimame, anapostahili pongezi tumpe na anapostahili lawama tumpe bila ya kuogopa tusiwe taifa la uoga"

Kwa upande mwingine, Mhe. Mbowe amesema hata Mwalimu Nyerere aliwaasa wasiwe taifa la uoga kwa kuwa watawaliwa na mtu ambaye hashauriki kwa jambo lolote.