Jumatatu , 27th Feb , 2017

Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ameweka wazi kuwamba Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ambaye ni baba yake mzazi pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa hawana matatizo yoyote kama jinsi watu wengi wanavyodhani

 

 Ridhiwani amesema kwamba licha ya maneno mengi  yaliyotokea kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 yaliyovuma zaidi baada ya jina la Lowassa kukatwa kwenye kinyang'anyiro cha kutafuta mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM,  watu wanatakiwa kutambua kuwa mchakato ule haukuwa jambo la Jakaya pekee bali yeye kama M/Kiti wa chama kazi yake ilikuwa ni kusimamia kupatikana kwa  kiongozi atakayependwa na watu.

"Mzee ni mtu wa kupita kwenye mitandao sana hata kejeli na matusi huwa anayaona lakini siyo mtu wa kuongea kabla muda wake haujaamua, kuna siku nilimwambia baba hapa ilipofika si sawa fanya kitu alinijibu akaniambia waache hao watu kwani bado hawajajua nguvu ya Rais, lakini ni mtu mwenye huruma mno". Alisema Ridhiwani Kikwete.

Kauli hiyo ya Ridhiwan imekuja muda mfupi baada ya kukutana na Lowassa katika uwanja wa Taifa, wakati wa mechi kati ya Simba na Yanga, ambapo alifanya naye mazungumzo pamoja na kupiga naye picha.

Ridhiwan Kikwete akizungumza na Edward Lowassa walipokutana katika dimba la Taifa

Ridhiwani ameendelea kusema kwamba baada ya baba yake kuona picha aliyopiga na Lowassa alimpigia simu na kumpongeza huku akimuasa asifikie mahala siasa ikawa vita.

Aidha Ridhiwani amebainisha kuwa familia yake (Jakaya Kikwete) ina mahusiano mazuri sana na familia ya Lowassa na kwamba huwa wanawasiliana mara kwa mara tofauti na inavyodhaniwa na watu.

Huenda hii ikawa ni harakati inayofanywa na Ridhiwan ya kuondoa hisia miongoni mwa watu kuwa Edward Lowassa na Jakaya Kikwete hawana maelewano mazuri.