Jumatano , 26th Nov , 2014

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali imependekeza kufukuzwa kazi kwa Waziri wa Nishati na Madini kutokana na kulipotosha bunge na taifa kwa ujumla kuhusiana na fedha ya akaunti ya Tegeta Escrow

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali imependekeza kufukuzwa kazi kwa Waziri wa Nishati na Madini kutokana na kulipotosha bunge na taifa kwa ujumla kuhusiana na fedha ya akaunti ya Tegeta Escrow pamoja na kuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Bwana Harbinder Sigh Sing Set na Bwaba Rugemalila katika ofisi za umma.

Akiwasilisha taarifa ya kamati kufuatia matokeo ya ukaguzi maalum wa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali katika akaunti ya Tegeta Escrow amesema waziri wa nishati na madini alifanya udalali huo akijua dhahiri kuwa Bwana Sethi hana uhalali wa kisheria kufanya biashara kwa jina la IPTL.

Kamati imependekeza waziri mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda kuwajibika kutokana na kauli zake za kuaminisha umma kuwa fedha zile siyo za umma kiasi kwamba vyombo vya habari ikiwemo gazeti la Daily News kuchapisha habari yenye kichwa cha habari kilichoandika hakukuwa na tatizo katika IPTL kauli inayoonesha alishindwa kutekeleza wajibu wake.

Aidha mwenyekiti wa PAC Zitto Kabwe amesema kamati hiyo inapendekeza mwanasheria mkuu wa serikali uteuzi wake utenguliwe na afikishwe mahakamani kwa matumizi mabaya ya ofisi yaliyopelekea serikali kupoteza mabilioni ya shilingi.

Kamati hiyo pia imetaja majina ya viongozi waliopata mgao wa fedha za Tegeta Escrow wakiwemo viongozi wa dini na baadhi ya watumishi wa idara na taasisi za serikali.