Jumatatu , 29th Mei , 2017

Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo amemvisha cheo kipya na kumuapisha Mkuu wa Jeshi la Polisi mpya (IGP) Simon Sirro Ikulu Jijini Dar es Salaam

Rais Magufuli akimuapisha Simon Sirro kuwa IGP

Baada ya kuapishwa (IGP) Sirro alikula kiapo cha uadilifu kwa uongozi wa umma na kuahidi kuwa atakuwa mzalendo kwa nchi yake ya Tanzania na mtii wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Nitakuwa muadilifu na mfano wa watumishi wa umma na watu wengine katika kukuza na kusimamia maadili, sitatumia cheo changu na wadhifa wangu kwa maslahi binafsi ya familia yangu, ndugu zangu au marafiki zangu, isipokuwa kwa maslahi ya umma. Nitalinda na kuitumikia rasilimali ya umma kwa maslahi ya umma, nitatekeleza majukumu yangu kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu na miongozo kwa maslahi ya umma. Sitaomba wala kushawishi kutoa au kupokea rushwa" alisema Sirro

Hafla ya kuapishwa kwa IGP Simon Nyakoro Sirro imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Gerson John Mdemu, Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Makatibu Wakuu wa Wizara na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Bw. Paul Christian Makonda.

IGP Simon Nyakoro Sirro amechukua nafasi ya Ernest Mangu ambaye atapangiwa kazi nyingine.