Alhamisi , 21st Mar , 2024

Tanzania na Ujerumani zimesaini makubaliano ya ahadi (commitment) ya msaada wa kiasi cha euro milioni 70 (sawa na shilingi bilioni 193.71) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania, ikiwemo sekta za maji, afya, maliasili, utawala bora na usimamizi wa sheria

Makubaliano hayo yametiwa saini Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya na  Mkuu wa Idara ya Afrika Mashariki, Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani, Marcus Von Essen.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, amezipongeza timu za wataalam wa nchi hizo mbili kwa kazi ya kuongoza majadiliano yaliyowezesha kukubaliana na kusainiwa kwa kumbukumbu za majadiliano hayo, ambazo zinaelezea ushirikiano wa nchi hizo kwa maendeleo ya wananchi wa Tanzania.

"Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatoa shukrani zangu za dhati kwa msaada huu ninawahakikishia kwamba, Serikali ya Tanzania itafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha kwamba fedha zinatumika kama ilivyokusudiwa," amesema Mwandumbya.

Aliongeza kuwa ahadi zilizotajwa zitasaidia miradi maalum ikiwemo  wa kupunguza migogoro baina ya  binadamu na wanyama , kiasi cha Euro milioni  tisa (9); mradi wa maendeleo endelevu ya mifumo ya hifadhi, kiasi cha euro milioni 15, mradi wa kuimarisha afya ya uzazi na kuwawezesha vijana  wa kike, kiasi cha euro milioni tisa  na  mradi wa kuimarisha mfumo wa Bima ya Afya wa kwa wote nchini Tanzania, kiasi cha euro milioni  tatu (3).