Jumamosi , 21st Jan , 2017

Balozi wa China hapa nchini Tanzania Dkt Lu Youging amepongeza hatua zinachukuliwa na serikali ya Tanzania katika kupambana na rushwa na ufisadi.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akipokea mfano wa hundi ya shilingi milioni 70 na laki nne kutoka Balozi wa China nchini, kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule ya msingi Chato

 

Dkt  Lu Youging ametoa pongezi hizo katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam katika sherehe ya maadhimisho ya mwaka mpya wa Kichina ambapo amesema serikali ya China na raia wake wanafurahishwa na hatua hizo kwa sababu zinalenga kuondoa na kukomesha rushwa na ufisadi kwani tabia hizo zikiachwa ziendelee zinachangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha utoaji wa huduma bora na za msingi kwa wananchi.

Akizungumzia mwaka mpya wa Kichina hapa nchini Balozi huyo amesema maadhimisho hayo ni muhimu kwa sababu raia Wachina na Tanzania wanajumuika pamoja katika kubadilisha mawazo na kutakiana heri na mafanikio kwa mwaka 2017.

Katika Maadhimisho hayo, Balozi wa China nchini Tanzania Dkt  Lu Youging amemkabidhi Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan mfano wa hundi ya shilingi milioni 70 fedha ambazo zitatumika katika ujenzi kwenye shule ya msingi Chato iliyopo mkoani Geita.

Baadhi ya washiriki wa maadhimisho hayo wakitembelea baadhi ya mabanda yaliyopo katika viwanja vya Mnazi Mmoja ikiwa ni sehemu ya maadhimisho yam waka mpya wa China leo jijini Dar es Salaam. China wanasherehekea mwaka mpya leo na kesho katika viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 11 jioni.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan amemhakikishia Balozi  huyo kuwa serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli itakuwa bega kwa bega na serikali ya China hasa katika uimarishaji wa sekta za biashara, utamaduni, elimu, afya  na masuala ya kijeshi kwa ajili ya maslahi na ustawi wa wananchi wa Tanzania na China.