Alhamisi , 29th Jan , 2015

Wafuasi 30 wa chama cha wananchi (CUF) leo wamefikishwa mahakamani baada ya kukamatwa na polisi juzi wakiwa katika maandamano kuadhimisha mauaji ya wenzao yaliyotokea mwaka 2001 visiwani Zanzibar.

Wafuasi 30 wa chama cha wananchi (CUF) akiwemo Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Uchaguzi na Bunge Shaweji Mketo na mkurugenzi wa mawasiliano Abdul Kambaya wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za mashitaka matatu likiwemo la kufanya mkusanyiko usio halali, ambapo wameshindwa kutimiza masharti na dhamana na kupelekwa rumande.

Wakili wa serikali Joseph Maugo amedai mbele ya hakimu Emilius Mchauro wa mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kuwa washtakiwa wanatuhumiwaa kwa mashtaka matatu ambapo shitaka la kwanza linalowakabili washtakiwa wote ambao wanatuhumiwa kula njama ya kufanya uhalifu.

Shitaka la pili linawakabili washtakiwa 28 ambao wanatuhumiwa kufanya mkusanyiko usio halali.
 
Imedaiwa kuwa walifanya mkusanyiko huo Januari 27 mwaka huu, wakiwa katika ofisi ya CUF iliyopo karibu na hospitali ya Temeke bila uhalali wowote walifanya mkusanyiko kwa nia ya kufanya maandamano kuelekea viwanja vya Zakhiem, Mbagala, Dar es Salaam.
 
Katika shitaka la tatu pia linawakabili washtakiwa 28, wanadaiwa kufanya mgomo baada ya katazo halali ambapo washtakiwa bila kujali tangazo lililotolewa na jeshi la polisi la kutokufanya maandamano wao walikaidi.

Washitakiwa wote wamekana kuhusika na tukio hilo huku wakili Maugo akidai upelelezi bado na pia kisheria mashitaka yao yana dhamana.

Mchauro amesema ili washtakiwa wawe nje kwa dhamana wanatakiwa wasaini dhamana ya sh. 100,000 na mdhamini mmoja wa kuaminika, lakini washtakiwa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande.
 
Washtakiwa hao watarudishwa mahakamani Januari 30 ili kuangalia kama wametimiza masharti ya dhamana, baada ya barua za wadhamini kwenda kuhakikiwa na upande wa mashtaka.
 
Nje ya mahakama hiyo kundi la wafuasi wa chama hicho walionekana wakihangaika huku na kule wakitaka kuwadhamini ndugu zao bila mafanikio na baada ya zoezi hilo kukwama walisubiri kuona wafuasi hao wanavyoondoka mahakamani hapo ambapo waliwasindikiza kwa nyimbo za chama hicho.