Ijumaa , 21st Jul , 2017

Rais Magufuli ameitaka kampuni ya Nyanza inayoshughulikia ujenzi wa barabara ya mkoani Kigoma kuanza kufanya kazi usiku na mchana kwa kuwa wapo baadhi ya wananchi hawajahi kuona lami maisha yao yote mpaka wanakufa.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo wakati akihutubia wakazi wa Kakonko mkoani Kigoma katika uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Kibondo mpaka Nyakanazi yenye urefu wa kilomita 50 kwa kiwango cha lami.

"Wananchi hawa wanahitaji barabara ya lami wameteseka tangu dunia iumbwe, wako watu hawajui rangi ya lami, wapo watu hapa wamezaliwa, wamezeeka hawajui rangi ya lami ikoje. Kwa sababu hawajawahi kuona barabara ya lami katika maisha yao, kwa hiyo nataka hii lami ianze na mjipange kweli mfanye kazi usiku na mchana", amesema Rais Magufuli. 

Pamoja na hayo Rais Magufuli amewaagiza makandarasi kufanya kazi ipasavyo na wasipofanya hivyo watachukuliwa adhabu kali zidi yao.

"Kwa bahati nzuri mimi kufukuza makandarasi ni kama kunywa chai, sasa asije akanirudisha kule nilipokuwa kwa sababu sasa ni Baba wa wote lakini nilipokuwa Waziri nilikuwa nafukuza tu, kwa kupitia bodi ya makandarasi nilikuwa nafuta wakandarasi na mimi nikuombe Prof. Mbalawa usiwe mpole. Makandarasi watakao kuwa wanafanya kazi hovyo hovyo, pole pole chukua 'action' ili kusudi kama kashindwa kufanya kazi ya ukandarasi akafanye nyingine hata ya kuvua samaki", amesisitiza Rais Magufuli.

Kwa upande mwingine, Rais Magufuli amewataka wananchi kibondo na kasuru wa mkoa wa Kigoma na watanzania wote kwa ujumla kudumisha ulinzi na usalama katika maeneo yao wanayoishi ili kupunguza au kumaliza kabisa matatizo ya kihalifu yanayotokea.