Jumatatu , 22nd Aug , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemtaka Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwenda wilayani Mpanda na kuangalia namna ya kuipanua hospitali ya Manispaa ya Mpanda ambayo inahudumia mkoa wote wa Katavi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea hospitali ya wilaya ya Mpanda akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya mkoa wa Katavi Agosti 21, 2016.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana katika ziara yake ya kikazi mkoani Katavi, ambapo pia alipata fursa ya kuitembelea hospitali hiyo.

Alisema hospitali hiyo ilijengwa mwaka 1957 kama zahanati ambayo kwa sasa inatumika katika kuwahudumia wananchi wate wa mkoa huo imezidiwa hivyo alimuagiza mkuu wa mkoa huo Meja Jenerali (Mstaafu) Raphael Muhuga kuharakisha ujenzi wa hospitali ya mkoa.

Aidha, Waziri Mkuu alisema kuwa wakati mkoa ukiwa kwenye harakati za ujenzi wa hospitali ya mkoa wilaya nazo zianze ujenzi wa hospitali za wilaya ili kuhakikisha sera ya Serikali ya kuwa na hospitali katika kila wilaya inatekelezwa.

Alisema kwa sasa madaktari na wauguzi wanaofanya kazi kwenye hospitali ya Manispaa ya Mpanda wamezidiwa kutokana na kuhudumia idadi kubwa ya wagonjwa kuliko uwezo wao. Hivyo amewataka madaktari na wauguzi wa wilaya ya Mpanda kuendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wenzao wa Manispaa.

Awali hospitali hiyo ilikuwa chini ya uongozi wa halmashauri ya Mpanda. Hospitali hiyo kwa sasa ipo chini ya Manispaa ya Mpanda hivyo Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa mkoa huo kuboresha huduma kwa kupeleka dawa na vifaa tiba vitakavyoweza hospitali hiyo kuhudumia wagonjwa wa mkoa.

Mkoa umetenga sh. bilioni 1.7 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya mkoa.

Waziri Mkuu, Kassim Majliwa na Mkewe Mary wakimtazama mtoto Nchambi Peter aliyeungua moto wakati walipotemblea hospitali ya wilaya ya Mpanda Agosti 21, 2016. Kulia ni Mam wa mtoto huyo, Dotto Makengele.