Jumatatu , 20th Mar , 2017

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye amesema endapo atashindwa kusimamia uhuru wa habari na vyombo vya habari nchini atakuwa hafai kubaki kwenye nafasi hiyo kwa kuwa atakuwa ameshindwa majukumu yake katika nchi huru.

Waziri Nape Nnauye

Nape ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumzia na kulaani kitendo kinachodaiwa kufanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, cha kuvamia chombo cha habari cha Clouds, akiwa na askari wenye silaha na kukifananisha kitendo hicho na kuinajisi taaluma ya habari.

Waziri huyo amesema amezoea kuona matukio kama hayo yanatokea kwenye nchi ambazo zimepinduliwa kwa bunduki lakini kwa nchi yetu si jambo jema kwenda kwenye vyombo vya habari na mabunduki mkononi.

"Tumezoea kuona matukio haya yanatokea kwenye nchi ambazo zimepinduliwa kwenda kwenye vyombo vya habari na mabunduki si sawa, kwa jambo hili tunataka kutenda haki tumsikilize Mkuu wa Mkoa ili tujue kwanini amefanya jambo hili". Alisema Nape

Kufuatia tukio hilo Waziri Nape ameunda tume yenye wajumbe takribani watano itakayoenda kumhoji Makonda na kutoa mrejesho wa kazi hiyo ndani ya masaa 24 ikiwa imeeleza sababu maalum kutokea kwa tatizo hilo.

Dkt. Reginald Mengi

Pamoja na hayo Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Dkt. Reginald Mengi amesema hawezi kutoa lawama kwa mtu yoyote mpaka pale ukweli utakapofahamika japokuwa ameonekana kukerekwa.

"Kwetu sisi hili ni jambo ni la hatari sana, linatuogopesha na linatishia maisha ya waandishi wa habari". Alisema Dkt. Mengi

Kwa upande mwingine Mengi amewasihi waandishi wa habari kutokuwa waoga kwa jambo lolote wanalopambana nalo ila wanachopaswa ni kufanya kazi kwa kufuata misingi iliyowekwa.