Jumatatu , 27th Feb , 2017

Kitendo cha Mbunge wa Arusha mjini kukaa rumande kwa zaidi ya miezi minne sasa pasipo kupatiwa dhamana kimemfanya Mbunge wa Kigoma Mjini Mh. Zitto Zuberi Kabwe kushindwa kuzuia hisia zake na kutaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iwajibishwe

Zitto Kabwe

Katika mtandao wake wa kijamii Mh. Zitto amedai kuwa kitendo cha  Mbunge huyo ambaye ni muwakilishi wa wananchi kunyimwa dhamana  ni siasa za ukomoaji ambazo zinajenga chuki kwenye jamii na chuki huwa zinazaa visasi.

"Haitoshi majaji kukemea Ofisi ya DPP, Mfumo wetu lazima uweke uwezo wa waendesha mashtaka wa aina ya kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini kuwajibishwa. Wanasheria tazameni namna ya kuwajibisha ofisi ya DPP kwa uonevu wa makusudi dhidi ya wananchi" Ameandika Zitto Kabwe

Mkurugenzi wa mashtaka (DPP), Biswalo Mganga

Hata hivyo kauli hiyo ya Zitto imekuja mapema leo baada ya  majaji watatu  kutoka mahakama ya rufaa kuitaka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali na DPP kuwa makini na kuwataka kuwashikilia watu kwa misingi ya kisheria na kuongeza kuwa haipendezi na haingii akilini mtu  kushikiliwa kwa miezi minne bila sababu kwa misingi ya kumnyima haki ya dhamana.

"Mnatufanya wanasheria wote hatuna akili na mnachafua mpaka  mahakama, kwa hali ya kawaida mtu mumshikilie kwa misingi ya kisheria, lakini katika kesi hii tumepitia jalada hatujaona kitu chochote cha kumshikilia Lema hadi leo na imetushtua sana". Alisema Jaji Stella Mugasha.