Jumatatu , 22nd Mei , 2017

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba ametoa agizo kali kwa kusema yeyote atakayebainika kumpa mwanafunzi mimba atachukuliwa adhabu kali dhidi yake na endapo mzazi naye atashabikia hilo naye atahukumiwa kwenye uovu huo pia.

Mhe. Mwigulu amesema hayo pindi alipokuwa anachangia hoja bungeni  Dodoma zilizokuwa zimemgusa na kusema imekuwa kawaida kwa viongozi pamoja na wazazi kutohangaika kujua ni namna gani ya kuwalinda wanafunzi wanaopata mimba, na badala yake wanahangaika kuhalalisha kuruhusu wanafunzi waliopata mimba kuendelea na masomo yao kama kawaida.

“Hatuwezi tukaipa dhambi jina zuri na baadae tukaitukuza. Watoto wengi wakipata mimba hatuangaiki ku-'protect' kwanini wanapata mimba, kwanini tusizuie wasipate mimba utotoni.Tunahangaika kutaka kuhalalalisha wapate mimba, Namimi nasema kama Waziri wa mambo ya ndani ya nchi atakayempa mimba mwanafunzi tutamkamata na atafika katika mikono ya sheria, mzazi atakaye shabikia mwanafunzi kupewa mimba na yeye atakuwa ameshiriki kwenye uovu wa hilo"- alisema Mwigulu

Pamoja na hayo Mhe. Mwigulu amesema kuwa mtoto mdogo aliyopo shuleni akaruhusu masuala ya kupata mimba basi atambue amekiuka maadili ya elimu, mila, imani pamoja na maadili ya sheria za nchi.