Ijumaa , 24th Mar , 2017

Mtayarishaji wa muziki Bob Maneck kutoka AM Records amesema anategemea kuachia kitabu chake kinachoelekeza na kufundisha masuala ya muziki hivi karibuni baada ya jambo hilo kushindikana mwaka 2016.

Mtayarishaji wa muziki Bob Maneck akiwa studio

Maneck amesema tatizo lilipolekea kushindwa kukitoa kitabu hicho ni kutokana na kutafuta waandishi waliobobea katika fani hiyo ili waweze kukiandika vizuri ili mradi kisiweze kumchosha msomaji mwenye nia ya kutaka kujifunza.

"Kwa jinsi nilivyopanga mimi na namna walivyoniambia wao sikutaka kitabu changu kiwe kirefu mpaka kimchoshe msomaji lakini jisni walivyoniambia kwamba kitabu kina kanuni zake, kuna vitu lazima vitimie ili kipitishwe na watu fulani ndiyo kikamilike kabisa" Alisema Maneck

Aidha 'Producer' huyo amesema wapo katika hatua za mwisho na mpaka kufikia mwezi wa sita kitakuwa kipo mtaani rasmi huku akifafanua maudhui ya kitabu hicho kuwa kitakuwa kimeegemea zaidi kwenye ujuzi wa 'production' ya muziki kwa sababu wengi wamekuwa wakifanya kazi hizo kama kipaji na siyo kusomea.