Jumanne , 28th Mar , 2017

Mkongwe wa bongo fleva Juma Kassim Nature 'Sir Nature' amekanusha vikali kulipwa na msanii Harmorapa katika wimbo wa 'Kiboko ya mabishoo' na kudai kwamba kijana huyo hana pesa za kumlipa na kusisitiza yeye alifanya kwa upendo tu.

Nature, Harmorapa

Akizungumza na eNewz ya EATV, Nature amesema kwamba alikubali kushiriki katika wimbo huo kwa sababu anaamini msanii huyo chipukizi ana uwezo mkubwa ikiwa ni pamoja na kuamini atafika mbali.

"Nikisema nimemlipisha Harmorapa pesa kwa ajili ya kolabo nitakuwa nakosea, mimi ni mtu mzima nilikubali kufanya wimbo na msanii yule kwa sababu ni mkali na anajua muziki pia na imani atafika mbali, hawezi kunilipa mimi, ana hela gani" - Juma Nature.

Katika hatua nyingine Nature kutoka TMK amesema yeye ameshakuwa mkongwe hivyo vijana kama kina Harmorapa wanapotokea kwenye ‘game’ inamlazimu kutoa sapoti ili hata watakapoondoka kuwe na watu wa kuendeleza muziki.

Aidha Nature amekanusha kusikia taarifa ambazo Harmorapa alidai kuwa amemlipa Nature kwa kolabo na kuongeza hizo taarifa kwa upande wake hazimkufikia rasmi.

Hata hivyo Harmorapa aliwahi kunukuliwa akisema siyo busara kwa wasanii wakongwe kuwalipisha pesa wasanii wachanga kwa kuwa ndiyo kwanza wanaanza kutafuta pa kutokea na kuweka wazi kuwa kwa upande wake alilazimika kumnunulia nguo Nature za kufanyia video ya ‘Kiboko ya Mabishoo’.