Jumatano , 4th Nov , 2015

Baraza la Sanaa Taifa BASATA limekanusha kupokea wimbo mpya wa msanii Roma Mkatoliki, ambaye alitoa taarifa kupitia ukurasa wake wa instagram kuwa anaenda kuwasikilizisha ili aweze kuuachia rasmi.

Akitoa taarifa hiyo kupitia kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, afisa habari wa BASATA Artides Kwizela,ameeleza kwamba kwamba hawajauona wimbo wa Roma na kitendo cha msanii kuandika kwenye mtandao haina tija kwani anajua taratibu za kufuata.

"Yani mtu kweli kukabidhi nyimbo anakabidhi kwenye ukurasa wake wa facebook! no, kwa sababu kuna utaratibu wake wa kuandika barua alafu ye mwenyewe Roma anaelewa hilo kuna procedure zake", alisema Kwizela.

Afisa habari huyo aliendelea kwa kusema kwamba ili wimbo upelekwe BASATA kukaguliwa ni lazima uwe umepitia COSOTA ili kupata haki miliki ya wimbo huo, kisha ndiyo uende BASATA.

"Wimbo unaanza na msanii mwenyewe amesajiliwa, akishasajiliwa wimbo anaouzalisha inabidi akausajili COSOTA uwe na copy right yake, baada ya kutoka hapo ndo uje kwenye procedure ya kusikilizwa kwamba una ownership tayari, kwa hiyo nyimbo nyingi ambazo wanazalisha wasanii unakuta wanapiga kelele wakati wimbo wake wenyewe hauna ownership hajaupeleka kokote", alisema Kwizela.

Roma alikuwa na mgogoro na BASATA kuhusu kufungiwa kwa nyimbo yake, hivyo alitoa taarifa kupitia ukurasa wake wa instagram kuwa ataenda kuwasikilizisha BASATA ili yasitokee kama yaliyotokea kwenye wimbo wake wa VIVA Roma.