Jumatano , 20th Sep , 2017

Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu imeisogeza mbele kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili aliyekuwa Kamishina Mkuu wa TRA, Harry Kitilya, Miss Tanzania 1996 Shose Sinare na mwenzao hadi Oktoba 5, 2017, kutokana na upelelezi kutokamilika.

Wakati akiahirisha kesi hiyo Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha amewaambia watuhumiwa kuwa upelelezi unakaribia mwisho hivyo wawe na imani na subira. Kitilya, Shose Sinare na Sioi Solomon wanashitakiwa kwa utakatishaji wa fedha kiasi cha dola milioni 6.

Upande wa mashitaka kupitia kwa wakili wa Serikali Mtalemwa Kishenyi mapema ulidai kuwa awali waliomba siku 14 ili kukamilisha upelelezi lakini muda huo haujatosha na kuomba siku zingine 14 ili kuja kueleza hali ya upelelezi wa kesi hiyo.

Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Masumbuko Lamwai umedai kesi hiyo imekuwa na dalili za kukomoana ambapo wateja wao wamekaa gerezani kwa takribani mwaka na nusu bila upelelezi kukamilika na inashangaza kuambiwa upelelezi bado.