Jumatano , 19th Jul , 2017

Prodyuza Mesen Selekta kutoka 'Defatality Music' ameunga mkono kauli ya Mkongwe  wa muziki Master Jay kwamba maprodyuza wengi Bongo ni wanafiki baada ya kushindwa kutekeleza azimio la kutorekodi wimbo chini ya Tsh. 1,000,000 kama ilivyopendekezwa.

Mesen amesema  kilichoongelewa na Master Jay kina ukweli kwani vikao vya maprodyuza vilikuwepo na walikuwa wanakutana na tayari ada ya malipo ilishajadiliwa ila kama imepuuzwa.

"Kinachokuja kutokea maprodyuza wanaokuja ni wengi, zamani studio zilikuwa chache kwa hiyo umoja wa kufanya maamuzi ulikuwa ni rahisi tofauti na sasa hivi studio ni nyingi, hivyo mtu anaangalia studio yangu ndio inaanza tukianza kurekodi wote milioni moja nitapataje wateja?, kuna muda mwingine mtu anapiga kishikaji,” alisema.

Hata hivyo Mesen ameongeza kwamba “Ni suala gumu lakini cha msingi maprodyuza watendewe haki katika malipo ya nyimbo na kila inapotoka prodyuza apewe asilimia yake ya malipo nadhani hiyo pia itasaidia,” amesisitiza.