Jumatano , 26th Jul , 2017

Baada Miss Tanzania 2001 Millen Magese  kupata mtoto wa kiume Julai 13 mwaka huu, rafiki wa karibu wa mrembo huyo anayejulikana kwa jina la Sophia Byanaku ameanika siri na tabia zilizokuwa zikisababishwa na ugonjwa uliomtesa zaidi ya miaka 20.

Millen Happiness Magese wakati akiwa mjamzito

Sophia ambaye aliwahi kuwa Miss Tanga 2001  amezungumza na  Nirvana ya EATV na kusema  kuwa Millen ameathirika kitabia na hali aliyokuwa nayo hata kumpelekea kuwa mtu mwenye hasira za mara kwa mara pasipo sababu.

"Matendo yake ya kuishi na watu yalikuwa yameathirika pia alikuwa mtu ambaye yupo 'So emotional. Kuna wakati alikuwa mtu mwenye hasira tu na ilihitaji watu wakaribu na  wanaofahamu ni kitu gani anapitia kuwa karibu naye ili kumfariji. Aliteseka sana lakini safari ambayo aliipambania imekuwa na matunda. ," alisema Sophia.

Bi Sophia Byanaku (Rafiki wa Millen Magese)

Bi. Byanaku ameongeza kuwa "Nimekuwa nikimshuhudia Millen akipata mateso haya tangu tukiwa watoto mpaka tunakuwa wakubwa. Furaha aliyo nayo kwa sasa imesababishwa na kutokuta tamaa kwake naimani atakuwa mama bora sana kwa mwanae Kairo. Lakini natamani kumuona akiendelea na kazi ya uanamitindo huku pia akiwa mama kwani naamini vyote anaweza kuvifanya kwa ubora zaidi.

Kwa upande wa kitaalamu Dokta wa maswala ya kina mama kutoka Dar es Salaam Dkt. Josephine Otieno amedai kitendo cha mtu aliyekuwa akisumbuliwa na hali ya 'Endometriosis' ni wazi atakuwa ametumia njia ya kitaalamu ijulikanayo kama 'In Vintro Fertilization' (Kupandikiza)"

'Kitaalamu kuna njia za kupandikiza kwa sababu kwa njia ya kawaida mtu mwenye matatizo ya 'Endometriosis' haiwezekani akapata mtoto. Njia ya IVF kwa hapa nyumbani inapatikana kwa gharama ya milioni 10 ambapo ni mara chache hutoa matokeo chanya kwa mara moja kwani wapo wanaopandikiza hata zaidi ya mara tatu mpaka nne"  alisema Dkt Otieno akizungumza na Nirvana.

Hata hivyo Millen aliwahi kukiri kwenye vyombo vya habari tofauti tofauti baada ya kuwa anabeba mimba kisha kutoka atafanya njia mbadala ya kuweza kufanikisha kupata mtoto.