Jumatatu , 27th Feb , 2017

Msanii Lulu Diva amefunguka kinachomkera katika kazi ya kuonekana kwenye video za muziki 'video queen' kuwa ni tabia ya wadada wengi wanaofanya kazi hiyo kujirahisisha kwa wanaume, jambo linalomfanya aichukie kazi hiyo hadi kuingia kwenye uimbaji.

Lulu Diva

Akiongea katika kipindi cha Planet Bongo cha East Africa Radio msanii huyo alionekana kukerwa na wadada hao kwa kuichukulia poa kazi hiyo na kusema hiyo ndiyo sababu ya wao kutolipwa pesa nzuri na wasanii.

"Nimetokea kutoipenda kazi ya 'Video Quen' kutokana na baadhi ya wadada hao kujirahisisha mno na hatimaye kazi hiyo kuonekana wahuni" Alisema Lulu 

Mrembo huyo ambaye kabla hajaingia kwenye tasnia ya uimbaji alikuwa ni miongoni mwa hao wadada wanaopamba video za muziki amesema misimamo yake ndiyo ilikuwa inampelekea kulipwa vizuri na kutolea mfano wa kazi mojawapo aliyofanya na Belle 9 kwamba alilipwa shilingi milioni 1.

Vilevile msanii huyo amewataka warembo hao waige mfano kwa wenzao kutoka nje ya nchi kazi wanavyozifanya ili waweze kupata malipo yao stahiki na siyo kuchafua ujuzi huo ambao mwisho wa siku watu wote wanaonekana hawana maana.