Ijumaa , 24th Mar , 2017

Msanii Dogo Janja ‘Janjaro‘ anayetamba na ngoma ya Kidebe amesema hawezi kuachia ngoma yake mpya kama jinsi ambavyo alivyokuwa amepanga kutokana na watanzania wengi kuwa ‘busy’ na masuala ya siasa.

Dogo Janja

Akiwa kwenye heshima ya Planet Bongo Janjaro amesema anafanya muziki wa biashara hivyo haoni sababu ya kutoa kazi mpya katika kipindi ambacho upepo wa kibiashara haujamnyookea.

 “Ukitaka kuuza vitumbua nyako na vikapata soko lazima uuze kipindi cha baridi lakini lazima uwe na chai ya moto, sasa kwa kipindi hiki upepo haujakaa kwenye target yangu maana kila nikiangalia, mara viongozi, huku siasa kwa hiyo nimeona ngoja nitulie nisubiri watanzania wakae sawa” Amesema Janjaro

Aidha Janjaro ameongeza kuwa hana haraka ya kuachia wimbo mpya tofauti na wakongwe wanavyopata ‘presha’ kwa sababu bado anadhani ana miaka mingi katika soko la muziki.

“Mimi bado nina kama miaka 25 ya kuimba muziki na nisipotee kwenye ramani hii, siwezi nikawa na presha kama watu wengine ambao umri umeenda, hata hivyo kwa vile hii ni biashara kila mtu ana target yake ya kuuza biashara yake, ila kwa sababu tayari nimesha ‘shoot’ hadi kichupa sina haraka mambo yatakaa sawa" alimaliza msanii huyo.

Jay Moe

Upepo huu wa siasa pia ulimkumba msanii mkongwe Jay Moe ambaye amelazimika kuachia wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la 'Nisaidie Kushare' wiki iliyopita baada ya kushindwa kuutoa tangu mwanzoni mwa mwezi wa pili kwa kuhofia kufunikwa na kiki za siasa.