Ijumaa , 24th Feb , 2017

Msanii mkongwe wa bongo fleva Khalid Mohamed 'TID' ameahidi kuwachukulia hatua watu wanaosambaza taarifa kuwa amepewa pesa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kama kivuli katika sekeseke la kutaja majina ya wanaohusika na dawa za kulevya.

Msanii wa Bongo Fleva: TID

Akizungumza katika kipindi cha 5SELEKT cha EATV, TID amefunguka na kusema kuwa yeye alikuwa ni muathirika wa dawa za kulevya na serikali ilimkamata kwa kosa la kutumia lakini ikaamua kumsaidia kwa kumfanya aachane na dawa hizo pamoja na kumpa nafasi ya kuelimisha vijana wenzake ambao bado wapo katika janga hilo.

TID ameonesha kushangazwa na kuumizwa na taarifa zinazoenea kuwa amepewa pesa ili ataje watu au ajitangaze, jambo ambalo amesema ni wivu wa baadhi ya watu wasiomtakia mema, na wanaotaka kumuona akiendela kutaabika kwenye matumizi ya dawa hizo.

"Watu wana ushahidi gani kama mimi Mh. Makonda kanipa mimi pesa au wanazungumza tu? mimi nataka huyo sijui Steve nani nani.....aseme kwamba aliniona nikipatiwa hizo pesa bila hivyo mimi nitamshtaki, unaituhumu serikali, bila ushahidi, hili ni kosa ambalo naweza nikampeleka mtu mahakamani" Amesema TID

Alipoulizwa kama sasa atakwenda mahakani, TID alijibu "Ndiyo nitakwenda Mahakamani..."

Msanii anayedaiwa kutoa kauli hiyo ya TID kupewa pesa ni Steve Nyerere, kupitia sauti za simu zilizosambazwa tangu juzi, zikionesha mtu anayedhaniwa kuwa ni Steve Nyerere akiongea na mtu anayedhaniwa kuwa ni Mama wa Msanii Wema Sepetu

TID akiwa ndani ya studio za EATV

Pia aliwajibu wanaodai kuwa amewageka "Unasema mimi nimekusnitch wakati wote tulikuwa ndani, nilipokuwa chini mbona ulikuwa unafurahi saivi nimetoka unasema nakusnitch?". Amehoji TID

TID amezidi kufunguka kwenye kipindi hicho kinachoruka saa 11:00 jioni na kuongeza kwamba madawa ambayo yeye alikuwa akiyatumia hayajamuathiri sana kiasi kwamba hana haja ya kumfanya yeye kwenda 'Sober House' kwa kuwa hayakumuathiri sana pia ni rahisi yeye kuyaacha kwa vile aliingia kwa mawazo ya kazi na mipango yake kutokwenda sawa na sasa ametoka huko yuko sawa.

Pamoja na hayo TID ameongeza kuwa yeye kutajwa katika orodha ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya na kufikishwa kituo cha polisi kumemuongezea mashabiki zaidi na kumfanya awe maarufu zaidi kutokana na simu za pole kutoka kwa mashabiki na wanahabari kuwa nyingi, pia kuandikwa na kuzungumzwa kwenye vyombo vyote vya habari.

Hii hapa ni sehemu ya mazungumzo ya TID na watangazaji T Bway na Shimii katika kipindi cha 5SELEKT