Alhamisi , 24th Jul , 2014

Chama cha kuogelea nchini Tanzania TSA kimetoa wito kwa wamiliki wa mabwawa na mahotel yenye mabwawa ya kuogelea kuhakikisha wanaajiri waokoaji wenye taaluma ya uokoaji ili kuepusha matatizo kwa waogeleaji pindi wanaposhindwa kuogelea

Baadhi ya waogeleaji wakichuana katika moja ya michuano ya kuogelea nchini.

Chama cha mchezo wa kuogelea Tanzania TSA kwa kushirikiana na uongozi wa michezo wa chuo kikuu na wamiliki wa mabwawa ya kuogelea nchini wanataraji kuandaa kozi maalumu kwaajili ya mafunzo ya uokoaji kwa waokoaji ambao wanafaya kazi ya kuokoa waogeleaji na wasio waogeleaji

Katibu mkuu wa TSA Noel Kihunsi amesema uamuzi huo umetokana na matukio ya watu kuzama katika maji hasa watoto na pia waokoaji kushindwa kuifanya kazi hiyo ipasavyo

Kihunsi ametolea mfano vifo vya watoto vilivyotokea katika Hotel ya Land Mark Mbezi Beach ambapo kama wangekua wameajiri waokoaji ambao wana taaluma ya uokoaji na wapo muda wote katika eneo la kuogelea pengine athali ya tukio hilo isingekua kubwa

Aidha Kihunsi amesema chuo kikuu kitasambaza barua kwa wahusika wote ili kufanikisha zoezi hilo na baada ya kozi hiyo watawafanyisha mitihani wanafunzi wote ili kupima uwezo wao kama wameelewa mafunzo hayo tayari kuanza kazi hiyo kwani wengi wanaofanya kazi hiyo ni watu ambao hawana taaluma hiyo ya uokoaji na ndio maana wanashindwa kukabiliana na tatizo la kuokoa pindi mwogeleaji anapozama au kushindwa kuogelea.