Jumatatu , 27th Feb , 2017

Beki wa Kimataifa wa klabu ya Simba na timu ya taifa Uganda juuko Murshid amejiunga rasmi na kikosi chake cha Wekundu wa Msimbazi mara baada ya kukosekana kikosi hapo kwa zaidi ya miezi miwili.

Juuko Murshid

Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu'  ndiye aliyetoa taarifa hiyo ambapo amesema hadi sasa tayari juuko amejiunga na kikosi cha Simba, na atakuwa ni mmoja kati ya wachezaji watakaoingia kambini kesho au kesho kutwa kwa ajili ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Mbeya City.

"Tayari Juuko amerudi, amerejea kazini na sisi tumempokea, maana tunaelewa matatizo aliyokuwa amepata kibinadamu , kwa hiyo hatua ya kwanza ni kumpokea lakini kama kuna mengine yataamuliwa baadaye, yuko na kikosi na ataingia kambini pamoja na wachezaji wengine" - Amesema Kaburu

Awali mchezaji huyo aliondoka nchini kurudi Uganda mwishoni mwa baada ya kupata matatizo ya kufiwa na watoto wake mapacha muda mfupi baada ya kuzaliwa, kabla ya kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya Uganda 'The Cranes' katika michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) iliyofanyika mwezi Januari nchini Gabon.

Mara baada ya michuano ile kumalizika, Juuko alitakiwa kujiunga na klabu yake ya Simba, lakini hakufanya hivyo hali iliyosababisha klabu hiyo kumtangaza kuwa ni mtoro kazini.