Alhamisi , 19th Feb , 2015

Shirikisho la Ngumi nchini BFT linatarajia kufanya shindano dogo la Ngumi mwishoni mwa mwezi huu kwa ajili ya kupata vijana 15 watakaounda kikosi cha timu ya Taifa kitakachokaa kambi ya muda mrefu kwa ajili ya kushiriki mashindano mbalimbali.

Akizungumza na East Africa Radio, Makamu wa Rais wa BFT, Lukelo Wililo amesema mpaka sasa wapo vijana 48 lakini katika vijana 15 kumi kati yao watakuwa ni katika kundi la awali na wengine watano watakuwa ni kundi la pili.

Wililo amesema, pamoja na kutafuta vijana hao, pia watatafuta kijana mmoja mwenye Umri kati ya miaka 17 na 18 atakayeliwakilisha Taifa katika michuano ya Jumuiya ya Madola ya Vijana yanayotarajia kufanyika Nchini Samoa Septemba mwaka huu.

Wililo amesema, kikosi chote kinatarajia kuingia kambini baada ya kumaliza mchujo ili kuweza kufanya maandalizi mapema kwa ajili ya michuano mbalimbali.