Jumatatu , 27th Feb , 2017

Mchezaji wa Simba Shiza Kichuya ambaye alitupia bao la ushindi siku ya Jumamosi katika mchezo kati ya Simba na Yanga ambapo timu hizo zilimaliza mchezo kwa Simba kuibuka na ushindi wa 2- 1, ameilazimisha Yanga kuwaangukia mashabiki zake.

Kutokana na matokeo hayo klabu ya Young Africans Sports Club kupitia katibu mkuu wake Boniface Charles Mkwasa, imeomba radhi wananchama wote pamoja na wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kwa matokeo mabovu iliyopata siku hiyo.

"Klabu inawaomba kuwa watulivu na pia inashukuru sana kwa utulivu mliouonyesha na kutii sheria zote kwenye mchezo wa Jumamosi. Matokeo haya tuliyopata ni ya kimchezo kikubwa ni kupambana na michezo iliyobaki mbele yetu na kuendelea kuwapa sapoti vijana wetu kwani bado tuna mashindano mengi na michezo mingi mbeleni. Tunaamini Mwalimu ameona mapungufu kwenye mchezo uliopita na atayafanyia kazi kuelekea michezo ijayo na tutafanya vizuri na kurejesha furaha yetu" alisema Boniface Mkwasa 

Hatua hiyo inafuatia mashabiki wa Yanga kuonesha kukwazika na timu yao kutokana na ukweli kwamba wao walianza kushinda katika dakika ya 5 ya mchezo na kumiliki mpira kwa zaidi ya asilimi 52 katika kipindi cha kwanza, huku timu hiyo ikipoteza nafasi mbalimbali za ushindi ambazo ilikuwa inazipata.