Jumapili , 15th Oct , 2017

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ameendelea kuonyesha umahiri wake akiwa uwanjani baada ya kuisaidia timu yake ya KRC Genk kuepuka kipigo kwenye uwanja wake wa nyumbani hapo jana.

Mbwana Samatta ambaye wiki iliyopita alikuwa hapa nyumbani kuitumikia Taifa Stars, amefanikiwa kutoa pasi iliyozaa bao la kusawazisha wakati timu yake ya KRC Genk ikitoa sare ya1-1 na Royal Excel Mouscron.

Mchezo huo wa ligi kuu ya Ubeligji ulipigwa kwenye Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk. Samatta alicheza dakika zote 90 ambapo pasi yake nzuri dakika ya 81 ilimsaidia Marcus Ingvartsen  kufunga bao la kusawazisha baada ya Genk kuruhusu bao la mapema kipindi cha kwanza kutoka kwa Dorin Rotariu  wa Royal Excel Mouscron.

Baada ya mechi ya jana, Samatta sasa ameichezea Genk mara 66 katika mashindano yote tangu Januari 2016, alipojiunga na timu hiyo. Genk inashika nafasi ya 10 ikiwa na alama 11. Vinara wa ligi hiyo ni Club Bruge ambayo ina alama 24.