Ijumaa , 24th Feb , 2017

Klabu ya Manchester United imepangwa na FC Rostov ya Urusi kwenye hatua ya 16 bora ya michuano midogo ya Ulaya, Europa League.

United itaanzia ugenini nchini Urusi, kwenye mchezo wa kwanza, Machi 9, kabla ya kurejea nyumbani Old Trafford, Machi 19.

Nayo klabu anayochezea Mtanzania Mbwana Alli Samatta, KRC Genk, itaanzia ugenini na Wabelgiji wenzao Gent Machi 9 kwenye Uwanja wa Ghelamco, mjini Gent.

Timu nyingine zilizopangwa kwenye hatua hiyo ni, Celta Vigo ya Hispania dhidi ya FC Krasnodar ya Urusi, wakati Schalke 04 itakuwa mwenyeji wa Mjerumani mwenzake Borussia Monchengladbach.

FC Copenhagen ya Denmark itakuwa nyumbani dhidi ya Ajax ya Uholanzi, wakati Lyon ya Ufaransa itaikaribisha Roma kutoka Italia, na Olympiakos ya Ugiriki ikishuka dhidi ya Besiktas ya Uturuki, na Apoel Nicosia ya Cyprus ikiwa mwenyeji wa Anderlecht ya Ubelgiji.