Jumatatu , 22nd Mei , 2017

Washambuliaji Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting na Saimon Msuva wa Yanga wameibuka wafungaji bora kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2016/2017 iliyomalizika Mei 20 mwaka huu.

Mshambuliaji wa Yanga, Saimon Msuva, akimpiga kanzu mchezaji wa Ruvu Shooting, Abdulahman Musa, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara

Kutokana na wachezaji hao kuibuka vinara kwa ufungaji ambapo kila mmoja amefunga mabao 14, watagawana zawadi ya mfungaji bora ambayo ni sh. 5,800,000 kwa kila mmoja.

Yanga imemaliza Ligi hiyo ikiwa bingwa kwa ponti 68 na kufunga jumla ya mabao 57, wakati Ruvu Shooting iliyomaliza katika nafasi ya saba kwa ponti 36 imepachika jumla ya mabao 28.

Watakabidhiwa zawadi hiyo katika hafla ya tuzo za Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2016/2017 itakayofanyika keshokutwa (Mei 24 mwaka huu) kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania {TFF}, Jamal Malinzi akilitolea ufafanuzi suala hilo amesema kuwa watapatiwa zawadi ya mfungaji bora kila mmoja kwa kuwa wamefunga mabao sawa katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kupitia ukurasa wake wa twitter Malinzi amesema "Kwa kuwa vijana wetu Abrahman Mussa na Simon Msuva VPL wamefunga mabao sawa 14 ni wafungaji bora na watapewa zawadi sawa ya Shilingi Milioni 5.8 kwa kila mmoja"