Jumatano , 19th Apr , 2017

Cristiano Ronaldo amesema Real Madrid, walistahili kuifunga Bayern Munich, kwa kuwa walicheza vizuri, na yeye mwenyewe kafurahia, kufunga hat-trick, katika ushindi wa mabao 4-2, mchezo wa marudiano hatua ya robo fainali ligi ya mabingwa Barani Ulaya.

Cristiano Ronaldo juu akishangilia na wachezaji wenzake na chini ni picha zinazoonesha mabao mawili ya utata wa offside aliyofunga nyota huyo.

Bayern, ambao walihitaji mabao mawili kusonga mbele, walikuwa wameongoza kupitia penati iliyofungwa na Robert Lewandowski dakika ya 53, kabla ya Ronaldo kujibu kufunga kwa kichwa kutokana na krosi ya Casemiro, kunako dakika ya 76.

Bayern walijibu sekunde 36 baadaye Sergio Ramos alipojifunga na kulazimisha mechi hiyo kuingia muda wa ziada.

Baada ya muda huo wa ziada, Ronaldo alifunga, mabao yake mengine mawili kunako dk za 105 na 120, na kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 100, kwenye michuano ya Ulaya, kabla Marco Asensio kuongeza bao la nne.

"Sisi ni washindi kabisa". Ronaldo alieleza tovuti ya Real Madrid.

"Kutunga mabao 6 dhidi ya timu kama Bayern siyo kazi nyepesi na tulistahili kuingia nusu fainali.

"Tulicheza vizuri sana, dhahiri ninafuraha kufunga goli zote tatu, lakini timu imekuwa vizuri."

Mreno huyo aliongeza: "Tulijitambua kuwa tunapaswa kucheza vizuri kwa sababu Bayern wanaweza kufunga mabao kutoka sehemeu yoyote ya uwanja na walithibitisha kuwa ni timu nzuri, lakini Real Madrid ni Real Madrid".

"Kwenye nusu ya kwanza tulikuwa na nafasi nyingi na tungeweza kufunga goli moja au mawili, pia kwenye kipindi cha pili pia.

"Yes, tuliruhusu mabao mawili, lakini Real Madrid imezoea kurudisha, tumeshinda na wote tunafuraha."

Kiungo wa kati wa Bayern Munich Arturo Vidal alitimuliwa uwanjani dakika ya 84, baada ya kupewa kadi nyekundu, kufuatia rafu mbaya kwa  Marco Asensio, jambo ambalo lilionekana kuathiri mwelekeo wa mechi hiyo.

Ronaldo naye alionekana kuwa alikuwa ameotea alipokuwa anafunga bao la pili la Real muda wa ziada.