Jumatatu , 28th Jul , 2014

Kocha Serengeti Boys Hababuu Ally amesema Morali waliyonayo wachezaji wake 19 walioondoka nchini kwenda Afrika Kusini wakiwa na viongozi 6 inampa matumaini ya kurejea nchini kifua mbele baada ya kuwatoa Amajambos ya Afrika Kusini

Kikosi cha Serengeti Boys kilichoondoka leo kwenda Afrika kusini.

Msafara wa watu 25 wa kikosi cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) umeondoka nchini hii leo kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Afrika Kusini (Amajimbos).

Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili itachezwa Jumamosi, Agosti 2 mwaka huu kwenye Uwanja wa Dobsonville uliopo Soweto, Johannesburg kuanzia saa 9 kamili mchana kwa saa za Afrika Kusini.

Ambapo kocha wa Serengeti Boys Hababuu Ally Omar amesema maandalizi ya timu yake kuelekea mchezo huo yamekamilika na amefanyika kazi mapungufu yote mabayo yalijitokeza katika mchezo wa awali ambao timu hizo zilitoka suluhu katika mchezo wa kwanza uliyofanyika Julai 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es salaam

Aidha Hababuu ametoa pongezi kwa shirikisho la soka nchini TFF kwa kufanikisha safari hiyo kitu ambacho kitaisaidia timu hiyo kupata muda mzuri wa mazoezi na kuzoea hali ya hewa ya Afrika Kusini hasa mji watakaochezea mchezo huo.

Naye nahodha Msaidizi wa Serengeti Boys Omar Wyne kwa niaba ya wachezaji wenzake amesema wako tayari kwa mchezo huo na morali yao iko juu kuhakikisha wanaibuka na ushindi huko ugenini

Wyne amesema walipata taabu katika mchezo wa kwanza kwakuwa walikuwa hawaja wasoma wapinzani wao lakini kwa sasa wamewaona na wanategemea kufanya vema na kinachopaswa ni watanzania kuwaombea dua ili wavuke kikwazo hicho na baadaye waingie mzunguko wa mwisho kwa kupambana na mshindi wa mchezo kati ya Misri na Sudan.