Jumatatu , 16th Jan , 2017

Mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast anayeichezea klabu ya wekundu wa Msimbazi Simba, Fredrick Blagnon amepelekwa kwa mkopo katika klabu ya Muscat ya nchini Oman kwa miezi 6.

Fredrick Blagnon

 

Klabu ya Simba imeweka wazi kuwa mshambuliaji huyo atakwenda nchini Oman kwenye klabu ya Muscat kwa muda wa miezi sita kwa ajili ya kulinda kiwango chake na baada ya hapo atarejea Msimbazi endapo hakutakuwa na makubaliano tofauti.

Tangu asajiliwe kikosin hapo, Blangnon amekuwa hana nafasi ya uhakika katika kikosi cha kwanza hali ambayo baadaye ilipelekea kuwekwa benchi moja kwa moja na kocha Mcameroon, Joseph Omog licha ya kusumbuliwa pia na majeraha ya mara kwa mara.

Katika mechi za ligi kuu alizoichezea Simba, amefanikiwa kufunga bao moja pekee, huku akiwa hajacheza mechi hata moja tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi, na hata kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Simba imekuwa ikihaha kupata 'mtambo wa mabao' tangu iachane wa Hamis Kiiza, kiasi cha kusajili washambualiaji kadhaa wa kimataifa msimu huu akiwemo Laudit Mavugo na Fredrick Blagnon, lakini bado hawajakidhi mahitaji, na mabao mengi yamekuwa yakifungwa kupitia viungo.

Hali hiyo imeilazimu kuongeza washambuliaji wa kitanzania katika dirisha dogo la usajili ambao ni Juma Luizio kutoka Zesco ya Zambia na Pastory Athanas kutoka Stand United, ambao wameua kabisa ndoto za Blagnon kupata namba hata ya ziada klabuni hapo.

Simba inakipiga na Mtibwa Sugar, JUmatano ya Januari 18 mjini Morogoro, na tayari imekwishaondoka Dar s Salaam kwa ajili ya mechi hiyo.