Jumamosi , 21st Oct , 2017

Mkimbiaji Usain Bolt ametangaza nia yake ya kujiunga na soka mwaka ujao na tayari vilabu kadhaa vimejitokeza kutaka huduma yake.

Bolt amesema kuwa alitamani kuanza kucheza soka mwaka huu lakini alipata majeraha ya misuli ya paja mwezi Agosti hivyo akashindwa kufanya mazoezi lakini anaamini mwaka 2018 ataanza vizuri maisha mapya ya soka.

“Nataka kuanza kucheza soka mwakani, kwasababu ni mchezo unaonivutia na nimesema hilo mara nyingi lakini mwakani nitaanza rasmi kuwa mwanasoka na tayari klabu nyingi zimeshajitokeza kutaka nizichezee”, amesema Bolt wakati anafanya mahojiano na FIFA.com.

Shabiki huyo wa kutupwa wa Manchester United hajaweka wazi ni klabu gani ataichezea hali ambayo imeacha maswali mengi kwasababu aliwahi kusema anatamani kuwa mshambuliaji wa Manchester United.

Bolt mwenye umri wa miaka 31 amestaafu kukimbia mwaka huu akiwa bingwa mara nane wa Olimpic pamoja na Ubingwa wa dunia mara 11 akitwaa medali za dhahabu.