Jumanne , 21st Nov , 2017

Makamu Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Michael Wambura amesema, kuna uwezekano mkubwa Bara la Afrika, likatoa idadi kubwa ya waamuzi katika fainali za michuano mikubwa hususani Kombe la Dunia.

“Waamuzi wa Afrika wana uwezo, Ninyi wakufunzi ni wa kufanya waamuzi wetu kuwa na uwezo zaidi. Ni Aibu kwa Bara kubwa kama Afrika lenye nchi wanachama 54 wa FIFA kuwa na waamuzi wachache katika fainali za Kombe la Dunia”, amesema Wambura.

Wambura ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua kozi ya Wakufunzi wa Waamuzi kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika.

Kozi hiyo itafanyika kwa muda wa wiki moja kwenye ukumbi wa ILO jijini Dar es salaam, ikiwafua waamuzi hatua ya tatu ‘Futuro III’ ambapo jumla ya washiriki 58 kutoka nchi 26 barani Afrika wanashiriki kozi hiyo.

Kozi hiyo ina wakufunzi sita akiwamo Carlos Henriques na Dominic Chiellens wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Wambura amesisitiza kuwa lazima kama bara waazimie kuwa na waamuzi wa kutosha katika fainali kubwa duniani.