Jumanne , 17th Jan , 2017

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara Yanga leo wanatupa karata yao mbele ya Majimaji ya Songea iLI kuweza kusaka pointi tatu zitakazowafanya kuwakaribia vinara, Simba SC.

Kikosi cha Yanga

Simba SC inaongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi 44 baada ya kucheza mechi 18, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 40 za mechi 18 pia.

Mbali na kuhitaji ushindi ili kujisogeza jirani na Simba, lakini pia Yanga wanatakiwa kushinda ili kurejesha furaha kwa mashabiki wao, baada ya timu hiyo kufanya vibaya kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Yanga ilipewa kipigo kichapo cha mabao 4-0 na Azam FC katika mchezo wa mwisho wa Kundi B kabla ya kutolewa kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi wiki iliyopita visiwani Zanzibar.

Kocha Mzambia, George Lwandamina amebeba kikosi kipana kikiongozwa na Makipa; Deo Munishi ‘Dida’, Ally Mustafa 'Barthez' na Benno Kakolanya.

Mabeki: Hassan Kessy, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Pato Ngonyani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan.

Viungo: Said Juma ‘Makapu’, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Juma Mahadhi, Deus Kaseke, Simon Msuva, Yussuf Mhilu, Geoffrey Mwashiuya.

Washambuliaji: Amissi Tambwe, Malimi Busungu na Matheo Anthony.