Bei ya vyakula na vinywaji baridi yapaa

Jumatano , 8th Jan , 2020

Mkurugenzi wa Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Ruth Minja, amesema kuwa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Disemba 2019, umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.3, kutoka asilimia 6.1 kwa mwaka ulioisha mwezi Novemba.

Picha ya Nafaka na vinywaji.

Hayo ameyabainisha leo Januari 8, 2020 wakati akitoa ripoti ya mwezi ya mfumuko wa bei, ambapo amesema, mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba 2019, umebaki kuwa asilimia 3.8 kama ilivyokua kwa mwaka ulioisha mwezi Novemba 2019.

Katika hatua nyingine Ruth amesema, wastani wa mfumuko wa bei wa Taifa kutoka mwezi Januari hadi Disemba 2019, umepungua hadi asilimia 3.4, kwa mwaka 2019, kutoka asilimia 3.5 kwa mwaka 2018.

Kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki, katika mfumuko wa bei unaonesha kuwa, mfumuko wa bei kwa nchi ya Kenya kwa mwaka ulioisha Disemba 2019, umeongezeka hadi asilimia 5.82, kutoka asilimia 5.56, huku nchi ya Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioisha mwezi Disemba 2019, umeongezeka hadi asilimia 3.6, kutoka asilimia 3.0.