Jumatatu , 2nd Jan , 2023

Baadhi ya wakazi wa manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wameishauri serikali kutafuta eneo jipya kwa ajili ya ujenzi wa soko kubwa na la kisasa na kukamilisha ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi ambacho ujenzi wake umeanza katika eneo la Kyakailabwa, lengo likiwa ni kufungua fursa za kiuchumi

Wakizungumza na EATV wakazi hao wamesema kuwa wanakubaliana na jitihada zinazofanywa na serikali katika kuhakikisha pato la mkoa linapanda, lakini endapo kutajengwa soko kubwa na kituo bora cha mabasi, itachangia uchumi kukua

"Soko letu hili tunalolitumia hivi sasa ni finyu, nashauri lipatikane eneo jingine kwa sababu wafanyabiashara tumekuwa wengi, kipindi kile tunaingia humu miaka kama 25 au 30 iliyopita tulikuwa kama 600 lakini kwa sasa tupo kama 2,000" amesema Ramadhan mfanyabiashara soko kuu

"Bado stand yetu hii inayotegemewa na wenyeji na wageni wanaokuja Kagera ni tatizo hasa mvua zikinyesha panajaa matope, nitafurahi sana endapo stand hii itajengwa maana itakuwa moja ya fursa na kivutio kwa wawekezaji wanaotamani kuja kuwekeza katika mkoa wetu" amesema Mwombeki mkazi wa manispaa ya Bukoba

Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila amesema kuwa katika mwaka huu 2023 kuna fursa nyingi za kiuchumi zitafunguka, na kuwataka wawekezaji kujitokeza kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwamo za kilimo, viwanda na ufugaji

"Fursa mojawapo ni mradi mkubwa ambao una zaidi ya shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kujenga stendi ya mabasi, masoko, barabara, kutengeneza taa na kujenga stendi ya malori, utagharamiwa na Rais mwenyewe kupitia World Bank, na fedha hizo Mungu akipenda haitazidi mwezi Machi, nina imani mambo yatakuwa mazuri" amesema Chalamila

Maombi ya wakazi hao ya kukamilishwa kwa kituo kikuu cha mabasi katika eneo la Kyakailabwa yemetolewa wakati mkuu wa mkoa akiwa ametoa kauli hivi karibuni kuwa yanakusanywa maoni ya wadau mbalimbali, ili kuona kama ujezi wa kituo hicho katika eneo hilo uendelee au litafutwe eneo jingine ambalo mabasi mengi yanatokea na hadi sasa majibu ya maoni hayo bado hayajatolewa.