Jumamosi , 28th Nov , 2020

Usafi wa mikono ambapo watu hutumia maji yanayotiririka na sabuni ni moja ya kanuni za afya za kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuhara na yale yanayoambukizwa kwa njia ya virusi.

Pichani Mama akimnawisha mikono mtoto ikiwa ni kufuata maelekezo yaliyotolewa Wizara ya Afya ikiwa ni mapambano dhidi ya Corona.

Hata maambukizi ya virusi vya Corona yalipoingia nchini Machi 16, mwaka huu, usafi wa mikono ilikuwa ni moja ya kanuni za afya zilizotangazwa kwa ajili ya kudhibiti maambukizi hayo.
 

Wahenga walisema “Kila janga huja na neema yake”, ikawa neema kwa wajasiriamali wanao tengeneza sabuni za maji, kwani bidhaa hiyo ilipata soko kubwa baada ya mahitaji ya bidhaa hiyo kuhitakijika kuanzia ngazi ya kaya na hata kwenye taasisi mbalimbali.

Wajasiriamali wanaotengeneza sabuni za maji jijini Mwanza ni miongoni mwa waliofikiwa na neema hiyo katikati ya janga la maambukizi ya virusi vya Corona.

 

Biashara wakati wa Corona

Edina Lyatuu, mkazi wa Majengo jijini Dodoma na mjasiliamali anayetengeneza sabuni za maji anasema kabla ya janga la ugonjwa wa Covid – 19 alikuwa anatengeneza na kuuza kiasi kidogo cha sabuni kwa wateja wachache nyumbani na maofisini.

“Lakini baada ya janga la corona kuingia nchini na wataalam kusisitiza umuhimu wa watu kunawa mikono kwa sababu kama sehemu ya kujikinga na maambukizi, mahitaji na mauzo yaliongezeka mara dufu,” anasema Edina

 

Anasema ilifikia wakati alilazimika kuzalisha na kuuza zaidi ya lita 60 za sabuni kwa mwezi.

“Kwa mwezi nilizalisha na kuuza galoni 15 za lita tano tano kwa bei ya Sh12, 000 kwa galoni moja,” anasema Edina

 

 Anasema kabla ya janga la Corona, bei ya galoni la lita tano la sabuni ya maji iliuzwa kwa Sh10, 000. Anasema ongezeko la uzalishaji, mauzo na kipato ilitokana na kuongezeka kwa idadi ya wateja waliokuwa wanahitaji sabuni kwa ajili ya kunawia mikono maofisini na majumbani.

Japo hakuwa na muda wa kutosha wa kuzalisha sabuni kwa wingi kutokana na kubanwa na majukumu ya kikazi, Edina ambaye pia ni mwajiriwa katika moja ya taasisi za Umma, anasema kipato chake kiliongezeka kipindi cha janga la virusi vya corona.

Mjasiliamali mwingine mkazi wa jijini Dar es Salaam, Elizabeth Aloyce anasema kabla ya corona alikuwa akiuza lita 20 pekee za sabuni ya maji kwa kipindi cha wiki mbili, kiwango lichoongezeka hadi kufikia lita 50 kila baada ya siku mbili hadi tatu.

 

“Biashara ilikuwa kubwa wakati ule maambukizi yalipoongezeka na wataalam kusisitiza umuhimu wa kunawa mikono na kuvaa barakoa, kuna wakati nilijikuta nikipata oda nyingi na kulazimika kufanya kazi usiku na mchana kukidhi mahitaji ya wateja,” anasema Elizabeth.

 

Bei ya malighafi kupaa

Siyo wajasiliamali wa kutengeneza sabuni ya maji pekee ndio walionufaika na janga la virusi vya corona, bali hata wafanyabiashara wanaouza malighafi za kutengeneza bidhaa hiyo nao walifaidika kwa kuongeza bei kutokana na ongezeko la mahitaji.
“Bei ya malighafi ya kutengenezea sabuni ya maji ilipanda kutoka Sh25, 000 ya awali hadi kufikia Sh40, 000 wakati wa janga la virusi vya corona. Hii ndiyo ilisababisha hata sisi kupandisha bei ya lita tano ya sabuni kutoka Sh10, 000 hadi Sh12, 000,” anafafanua Elizabeth

 

 Hata hivyo, bei ya malighafi ya kutengenezea sabuni ya maji tayari imeshuka na hivyo kuwafanya wajasiliamali nao kupunguza bei ya bidhaa hiyo kwa wateja wao.

Malighafi ya kutengeneza sabuni Kwa mujibu Elizabeth Aloyce, malighafi inayohitajika kutengeneza bidhaa hiyo ni Kemikali aina ya Salfonic kwa ajili ya kuuwa bacteria, Slace kwa ajili ya kutengeneza mapovu, griselini kwa ajili ya kulainisha mikono, chumvi ya mawe, marashi, rangi pamoja na maji.

 

Biashara baada ya covid 19
Baada ya maambukizi na wagonjwa wa covid 19 kutangazwa kupungua nchini, wajasiliamali wa kutengeneza sabuni za maji wamejikuta kipato chao kikipungua kutokana na idadi ya wateja na mahitaji kupungua.

“Baada ya janga la covid 19 kutangazwa kumalizika, uzalishaji, mauzo na hata faida imepungua kwenye biashara ya sabuni yaaji,” anasema Edina Anasema tofauti na wakati wa corona alipouza hadi lita 50 kwa siku mbili hadi tatu, hivi sasa anauza kati ya lita tano hadi 10 pekee kwa siku.

 

Changamoto za Wajasiriamali wadogo

Kuongezeka kwa mahitaji na gharama za maisha ni changamoto nyingine wanayokumbana nayo wajasiliamali kabla, wakati na hata baada ya ugonjwa wa covid 19 ambapo mjasiliamali Bertha Mwaluko, mkazi wa Gongo la Mboto jijini Da es Salaam anasema wanakabiliana nayo kwa kuanzisha shughuli zingine za kujiongezea kipato.

“Wanawake wajasiriamali wanaotengeneza sabuni za maji pia wanajihusisha na biashara zingine ikiwemo biashara ya kununua na kuuza bidhaa za chakula magengeni,” anasema Bertha

 

 Funzo wakati wa covid 19

“Kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika usiku na mchana kumudu mahitaji ya wateja ni moja ya funzo muhimu niliyoipata wakati wa kipindi cha corona,” anasema Lucky Protas, mjasiriamali, mkazi wa mtaa wa Uhuru jijini Mwanza

 

Lucky ambaye pia anatengeneza na kuuza sabuni za maji anataja funzo lingine alilopata wakati wa corona ni umuhimu wa wajasiliamali kushirikiana kwa kuweka pamoja mitaji na ujuzi ili kuzalisha bidhaa kwa wingi kukidhi mahitaji ya wateja.
 

Utamaduni wa kunawa mikono

 

 “Japo janga la virusi vya corona limeisha, bado naamini jamii yetu inatakiwa kudumisha mwamko wa kunawa mikono kama njia ya kukabiliana na magonjwa mengine ya kuambukiza yanayotokana na uchafu wa mikono,” anasema Elizabeth

 

Kauli hiyo inaungwa mkono na mjasiriamali Hadija Mussa ambaye pia ni Ofisa Muuguzi akiwataka Watanzania kuendelea kunawa mikono kwa maji safi na sabuni kwa sababu inasaidia kuondoa na kuuwa vijidudu vinavyoambukiza maradhi, hasa kuhara na magonjwa ya tumbo.

Ili kujikinga na maradhi, inashauriwa kila mtu kunawa mikono kwa maji safi na sabuni kabla ya kuandaa chakula, kabla ya kula na baada ya kujisaidia au kumtawaza mtoto. Wakati wa kupiga chafya na kukohoa, watalaam wa afya wanashauri watu kuacha kutumia viganja vyao vya mikono, badala yake watumia sehemu ya mbele ya kiwiko.