Alhamisi , 11th Jun , 2020

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetoa idhini ya utambuzi ya miaka 3 kwa Shirika la ndege la Precision Air Tanzania Plc, inayotambua na kuruhusu uzalishaji wa Barakoa.

Moja ya ndege za Shirika la ndege la Precision Air

Hatua hiyo imekuja baada ya Precision Air kuwasilisha maombi kwa mamlaka hiyo na kufudhu ukaguzi uliofanywa ili kutathimini ubora na wa bidhaa (Barakoa) na mazingira ya kiwanda cha uzalishaji.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Precision Air Bw. Patrick Mwanri amesema shirika hilo litaanza uzalishaji wa  Barakoa kwa ajili ya wafanyakazi lakini pia wakitarajia kuziingiza sokoni kwa ajili ya kuuzwa kwa umma.

“Tunaishukuru TMDA kwa kutupatia kibali, kwani hatua hiyo itatuwezesha kuzalisha Barakoa zetu wenyewe tukiwa tunalenga kuwalinda wafanyakazi pamoja na abiria wetu. Tumezingatia muongozo wa Serekali kupitia wizara ya Afya na ile ya Utalii juu ya kufanya shughuli zetu huku tukiwalinda wafanyakazi na abiria wetu dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona.” Ameeleza Bw. Mwanri.

Bw.Mwanri amefafanua zaidi kuwa awamu ya kwanza ya uzalishaji wa Barakoa hizo utalenga kwanza wafanyakazi wa Precision Air na kwamba awamu ya pili itahusisha uzalishaji mkubwa kwa ajili ya kuziingiza sokoni kwa gharama nafuu ili kusaidia katika mapambano dhidi ya ugonywa wa korona.

Katika hatua nyingine,kuanzia tarehe 15 juni shirika la ndege la Precision Air linatarajia kurejesha safari zake za Zanzibar, Arusha  na Bukoba ambazo hapo awali zilipunguzwa kutokana na kushuka kwa abiria kulikosababishwa na hofu dhidi ya Corona.

Precision Air ni shirika la umma lililoanzishwa mnamo mwaka 1993 na linatoa huduma za usafiri  wa anga kwenda sehemu mbali mbali ndani na nje ya nchi. Safari zake huanzia makao yake makuu Dar es Salaam, kuelekea Arusha, Kilimanjaro, Serengeti, Mtwara, Kahama, Bukoba, Mwanza, Zanzibar, Tabora, Serengeti, Dodoma, Nairobi na Entebbe. (Safari za Nairobi na Entebbe zikiwa zimesitishwa kwa muda kutokana na makatazo yaliyotolewa na nchi husika kama njia za kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa wa  Corona.) Huduma nyingine zinazotolewa na shirika la Precision Air ni pamoja na huduma za usafirishaji mizigo.