Jumatano , 10th Jul , 2019

Kampuni ya Mawasiliano ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania, imeanzisha huduma inayomuwezesha mteja, kuongezewa muamala wa pesa pindi anapopungukiwa.

Mkurugenzi wa M-pesa Epimark Mbeteni.

Akizungumza Jijini Dar Es Salaam, Mkurugenzi wa M-pesa Epimark Mbeteni amesema, huduma hiyo imekuja kwa kushirikiana na benki ya TPB, na kwamba ushirikiano huo utaweza kutatua matatizo ya kifedha yanayojitokeza.

''Hii ni huduma ambayo itaweza kumsaidia mteja kukamilisha muamala uliopungua, wakati wa kununua Luku, kutuma pesa, au wakati wa kununua bidhaa mbalimbali''.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Benki hiyo, Mkurugenzi wa vihatarishi wa TPB, Mosses Manyata amesema, huduma hiyo iliyopewa jina la Songesha na M-pesa, ni mtatuzi wa matatizo ya ghafla kwa mteja, wakati wa kutuma pesa ama kulipia bili mbalimbali.

Hii ni mara ya pili sasa kwa Kampuni ya Vodacom, kuungana na Benki hiyo, na kutoa huduma inayohusisha na kugusa maisha ya watanzania wengi.