Jumatatu , 3rd Oct , 2022

Waziri wa Madini Dkt. Dotto Biteko amewaonya wachimbaji wa Dhahabu wanaotorosha madini hayo kwa kupunguza thamani yake kukiona cha moto kwani serikali imejenga miundombinu ya kuuzia dhahabu na imepunguza gharama ya tozo zilizokuwa zinawafanya wachimbaji wakwepe masoko ya ndani.

Waziri wa Madini Dkt. Dotto Biteko

Dkt. Biteko ameyasema hayo wakati anazindua maonesho ya tano ya Teknolojia ya uwekezaji kwenye sekta ya Madini yaliyofanyika viwanja vya bombambili mkoani Geita na kuwaonya wachimbaji na wauzaji wa Dhahabu kuacha mara moja utoroshaji huo.

"Umetoka kwenye utoroshaji wa kubeba Dhahabu ukaificha ukaenda kuuza mahali pengine umekuja utoroshaji mwingine wa kisayansi, unashusha purity ya Dhahabu, kama Dhahabu ina 90% basi unashusha inakuwa 87% unaiba 3%, nataka niwaambieni wanaofanya jambo hili mambo mawili wanayatafuta, wanatafuta a wanatafuta umaskini, sheria ya madini inaeleza dhahiri mtu yeyote atakaefanya kitendo cha namna hiyo kwanza madini hayo yaliyofanyiwa ujanja yatataifishwa pamoja na vyombo vyote vibavyotumika kuyasafirisha na utakapopelekwa mahakamani utapigwa faini mara tatu ya thamani ya madini hayo," amesema Waziri Biteko. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigella anasema kupitia maonesho hayo wamejiandaa kutoa nafasi kwa wafanyabiashara ambao wapo tayari kuweka miundombinu ya kudumu kwenye viwanja hivyo.

"Tumejipanga kuanzia mwakani tunataka tuweke utaratibu mzuri wale ambao watataka kuweka miundombinu  ya kudumu tuweze kugawa  maneneo waweze kuyajenga hapa ili shughuli za maonesho zisibaki kufanyika kwa mwaka mara moja peke yake tuweze kuwa na shughuli za utangulizi kabla ya kuwa na shughuki za maonesho zinazofanyika mwezi wa nane au mwezi wa tisa",amesema Martine Shigela. 

Baadhi ya washiriki wa maonesho hayo wanasema waliona umuhimu wa kushiriki ili waweze kutoa Elimu kwa wananchi juu ya taasisi zao.