“Wagombea muwe makini tusilaumiane”- NEC

Jumamosi , 1st Aug , 2020

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imevitaka vyama vya siasa kuchagua watu makini ili kuepusha migogoro baina yao na Tume, pindi wanapotakiwa kukamilisha mchakato wa kupitisha majina ya wagombea.

Mwenyekiti wa Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage, wakati akizungumza na wadau wa vyama hivyo leo Agosti 1, 2020, jijini Dar es salaam, ambapo wamejadili Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, na mambo ya kuzingatiwa.

Amesema kuwa fomu za uteuzi zitaanza kutolewa Agosti 5, 2020, kwenye makao makuu ya ofisi za Tume jijini Dodoma kwa wagombea wa kiti cha Urais huku Wabunge na Madiwani watafuata fomu hizo katika makao makuu ya Halmashauri ya Majimbo na Kata husika.

“Fomu zitaanza kurejeshwa muda wowote pindi mgombea anapomaliza kujaza kwa usahihi hadi Agosti 25 saa 10 jioni, ambayo ndiyo itakuwa siku ya uteuzi, naomba mjaze kwa usahihi bila dosari yoyote ili usijekosa sifa na usiteuliwe na kuanza lawama”, amesema Jaji Kaijage.

Jaji Kaijage ameongeza kuwa, “Wale wote wenye malalamiko na tume tunaomba mtuletee wenyewe tutayafanyia kazi, ila sio kulalamikia mitandaoni hatutajihusisha na malalamiko ya mitandaoni”.

Ameongeza kuwa Tume imekamilisha uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ambapo waliojiandikisha ni zaidi ya Milion 29 na kusisitiza kampeni za uchaguzi kwa Zanzibar zitaisha Oktoba 26,2020 ili kupisha upigaji kura ya mapema ya Rais wa Zanzibar, Mwakilishi na Diwani.