Alhamisi , 16th Jul , 2020

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, pamoja na wanachama wengine wamemuomba aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe, kuchukua fomu ya kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao, kupitia chama hicho.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, ambaye kwa sasa ni mwanachama wa ACT Wazalendo.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Julai 16, 2020, katika hafla ya chama hicho kwa ajili kumkaribisha rasmi Membe ndani ya chama, kwa kuwa Membe ni kiongozi imara na hayumbishwi na kwamba chama hicho kimevuna kumpata yeye na kitapaa.

"Membe ni maarufu nchini Tanzania na Dunia inamtambua, na ndiyo maana wanamuogopa, chama chetu kama kilikuwa kinajulikana Kenya na Uganda sasa kinajulikana Dunia nzima, Membe wamekusikia sana lakini kuna ujumbe wa wanachama wenzako, wanakuomba uchukue fomu ya kugombea Urais hata ukipenda chukua leo leo", amesema Maalim Seif.

Awali akizungumza, Membe amesema kuwa ameamua kusonga mbele na chama cha ACT Wazalendo na kamwe hatorudi nyuma.

"Kuna watu wameniuliza wewe hautakuwa kama yule wa kwenda na kurudi nyumbani, hapa mimi ndiyo nyumbani kwangu, mimi ni mbele kwa mbele, mazingira yaliyonifanya mimi niingie ACT ni tofauti kabisa yaliyomfanya mwenzangu akaenda kule na kurudi", amesema Membe.