Jumamosi , 17th Dec , 2022

Mtu mmoja ajulikanaye kwa jina la Jovitus Kazimoto (46)  ambaye ni mfanyabishara anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Mwanza kwa kukutwa na shehena ya mifuko ya plastiki viroba 45 inayosadikiwa kuingizwa nchini toka nchi jirani kwa kupitia njia za maficho

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amesema mifuko hiyo iliyokatazwa na serikali imekutwa ndani ya gari namba T 421 ADM Canter Mitsubishi lililokuwa limeegeshwa katika eneo la Chamabanda wilayani Sengerema

‘Tulipokea taarifa kutoka kwa wasiri wetu waliotapakaa maeneo mbalimbali wakatufahamisha kwamba kuna shehena imebebwa kwenye gari inayosadikiwa kuwa ni paketi za plastiki ambazo zimeshapigwa marufuku na serikali kwamba zilikuwa zimeingizwa kutoka sehemu moja ambayo bado tunaifuatilia nchi Jirani na kuingia nchini kwetu kwa ajili ya matumizi katika mkoa huu na pengine mahala pengine wakati tayari zimekwishapigwa marufuku na serikali"

"Baada ya kupata taarifa hizo tukachukua hatua za haraka na kaunza kufuatili tukaweza kukamata gari aina ya Mitsubishi canter T 421  pamoja na aliyekuwa analiendesha Juvitus Kazimoto’

Aidha kamanda Mutafungwa amesema upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani

"Huyo dereva ameshikiliwa hapa katika kitengo cha upelelezi lakini gari pamoja na vielelezo nilivyovitaja hapa vimeshikiliwa pia tunaendelea kufanya upelelezi ili kubaini wale wote wanaohusika nah ii biashara ya kusafirisha au kuuza mifuko ambayo serikali imepiga marufuku tunaendelea pia kushirikiana kwa karibu na mamlaka nyingine za serikali kama NEMC kufanya uchunguzi kwa pamoja kuhakikisha mtuhumiwa anachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria"

Katika hatua nyingine kamanda Mutafungwa amewataka wakazi wa jiji la Mwanza kuendelea na maandalizi ya sikukuu ya Krismas na mwaka mpya kwani jiji hilo lipo salama

‘Nichukue nafasi hii kuendelea kuwakumbusha wakazi wa jiji la Mwanza kuendelea na maandalizi ya sikukuu yam waka mpya na krismas niwaambie kwamba jeshi la polisi tunaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kufanya doria za mara kwa mara na kuwashughulikia wahalifu"