Ijumaa , 4th Dec , 2020

Katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana nchini, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimezindua programu ya kuwajengea uwezo wanafunzi wanaohitimu elimu ya juu ili kuweza kukidhi vigezo katika soko la ajira.

Dkt. Jakaya Kikwete Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa programu hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Gen Empower Mkuu wa Chuo hicho, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema kuwa programu hiyo itaongezea vijana ujuzi na maarifa ili kuweza kupata ajira na kujiari wenyewe badala ya kusubiria ajira.

Isiwe fahari kwa wanafunzi kukaa Vyuoni kwa miaka mitatu au zaidi na kuishia kuvaa majoho na kurejea majumbani, programu hii tuna imani itakuwa chanzo cha kuondoa na kumaliza kabisa tatizo la Ajira nchini", amesema Dkt. Kikwete.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa William Anangisye amesema kuwa chuo hicho kina mikakati ya kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi na moja ya mikakati iliyowekwa ni kuhakikisha kupitia programu hiyo wanaanzisha kituo cha ujasiriamali kinachowajengea maarifa vijana kupata elimu ya ujasiriamali na ajira.

Naye Meneja Programu kutoka Gen Empower Amani Shayo, amesema kuwa wameamua kuwapa wanafunzi taaluma ya uelewa wa kuweza kujiajiri na mpaka sasa tayari wana wanafunzi 270.